0
Serikali inatarajia kuziboresha shule za msingi inazomiliki ili ziweze kuwa na hadhi sawa na zile za mchepuo wa kiingereza zinazomilikiwa na watu binafsi, hatua ambayo inalenga kufuta dhana ya shule hizo kubezwa kwa madai ya kutokuwa na kiwango bora cha utoaji elimu ikilinganishwa na shule hizo za binafsi.

Naibu Waziri wa nchi Ofisi wa Makamu wa Rais Charles Kitwanga ametangaza mpango huo wa Serikali wakati akizungumza na wazazi wanaojiandaa kuanza safari ya kuwasomesha watoto wao kidato cha kwanza baada ya kuhitimu elimu ya darasa la saba katika shule ya Msingi Nyamalango iliyopo kata ya Mkolani wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

Amesema uboreshaji huo utahusisha ukarabati wa majengo, ujenzi wa maktaba za kisasa pamoja na uwekaji wa nishati ya Umeme huku akiziagiza kamati za shule kuzingatia ulipaji wa gharama za umeme kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kukatiwa nishati hiyo, lengo likiwa kuondoa matabaka yaliyoanza kujitokeza katika mfumo wa elimu nchini.

Post a Comment

 
Top